
Kabla ya kuingia rasmi katika mwendelezo wa mada yetu ambayo ilianza wiki iliyopita juu ya mwanaume sahihi wa kumpa moyo wako, napenda kutoa changamoto kwenu marafiki zangu.
Siku inapoondoka inakuwa imekwenda, haiwezi kurudi tena. Umakini katika kila kitu unachokifanya katika maisha ni jambo muhimu sana marafiki. Hebu jiulizeni, tukiwa tumeshaanza nusu nyingine ya mwaka, mmefanya nini?
mna mafanikio gani katika kipindi cha nusu mwaka kilichopita?
Je, mnaishi mkiwa na mipango ambayo mnaitekeleza au mnakwenda tu, mradi siku zinakwenda? Ishini kwa mipango rafiki zangu, siku ikiondoka, hakuna nyingine tena kama hiyo.
Hata katika mapenzi, unapaswa kujiuliza, umefanya nini kwa mpenzi wako? Je, umekuwa hodari wa kupanga wenzi wengi au umedumu na yule uliyekuwa naye tangu mwaka jana? Makosa madogo yanayotokea katika uhusiano wenu, umeyaweka sawa au ndiyo umeona uamuzi wa kuachana ni bora zaidi?
Kuwa na wapenzi wengi si ujanja, kubadilisha wenzi kila siku si kigezo cha kukufanya uonekane mwerevu! Rafiki yangu, lazima uwe makini kuhakikisha uhusiano wako unaendelea kuwa wenye nguvu kadiri siku zinavyozidi kwenda mbele.
Wale mliopo kwenye ndoa, mnatakiwa kufahamu kwamba ugomvi si kitu cha kuendekeza. Kupishana kiswahili ndani ya nyumba ni jambo la kawaida, muhimu hapa ni kuangalia namna mnavyokabiliana na changamoto hizo na maisha kuendelea kama kawaida.
Acha usiri kwa mwenzi wako, kama mnaishi ndani ya ndoa ni lazima muwe wamoja mkielezana ukweli wa kila kinachotokea katika maisha ya kawaida. Kama kuna jambo la maendeleo unataka kulifanya, usifanye kimya kimya, kaa chini na mwenzako mjadiliane.
Kwa kufanya hivyo, uhusiano wenu utazidi kuwa wenye nguvu zaidi na mafanikio makubwa yatakuwa ndiyo zawadi ya mapenzi yenu. Rafiki zangu, hizo ni dondoo tu za kumaliza nusu ya mwaka, sasa tuendelee na mada yetu.
Si kila mwanaume anaweza kuwa mume, wengine wana tabia chafu ambazo kama hutakuwa makini utagundua ukiwa tayari umeshaingia kwenye kifungo cha ndoa, ambapo hapo sasa hutaweza kutoka tena.
Kama mtakumbuka vizuri, wiki iliyopita nilianza kwa kuelezea baadhi ya vigezo muhimu vya kuzingatia kwa mwanaume ambaye anafaa kuwa wa maisha. Nilisema aliye mkweli, anayekujali na mwenye msimamo.
Kila kipengele nilikifafanua kwa marefu na mapana, leo tunamalizia vipengele vilivyosalia, nikiamini kwamba vitakupa tiba katika kufanya maamuzi sahihi kwenye uhusiano wako.
ANAYESHAURIKA
Mwanaume ambaye anafaa kuwa baba bora wa familia ni yule ambaye anakubali mawazo ya mwenzake. Anakubali ushauri. Siku zote amekuwa mkweli kwako, anakubayanisha mali zake pamoja na biashara anazofanya.
Haoni vibaya kukufundisha juu ya kuendesha mali zake. Inapotokea unamshauri, hukusikiliza kwa umakini na kuyafanyia kazi mawazo yako. Hata kama akiona ushauri wako si wa busara sana au akawa na mashaka nao, hutulia na kupima maneno yako kwa umakini kabla hajayafanyia kazi.
Ni vema mwanaume ashaurike (inapobidi) ili asifanye madhara katika maamuzi ya familia kwa kusingizio cha ubaba ndiyo kichwa ca familia. Dalili za udikteta kama anazo utaziona mapema sana katika kipindi cha urafiki wenu.
Kama ana tabia hiyo ni wazi kwamba hata mkiwa kwenye ndoa, utakuwa msindikizaji tu; mawazo yako hayatathaminiwa na mchango wako hautaonekana.
ANAJALI NDUGU ZAKO
Hapa nazungumza zaidi na wale ambao uhusiano wao tayari unajulikana. Wazazi wa pande zote wanaufahamu. Kama ndivyo ni lazima mwanaume wako awe na upendo na ndugu, jamaa na marafiki zako.
Kuna msemo wa Kiswahili unasema `ukipenda boga, penda na lake’ na msemo mwingine unaofanana na huo unasema `unapopenda jipu penda na usaha wake’ kwa wakati mmoja, misemo hii inasisitiza upendo.
Kwamba kuna vipimo kadhaa vya upendo lakini moja ni kumwangalia kama ana upendo kwa ndugu zako. Mwanaume huyu mara zote huulizia hali za wazee wako pamoja na ndugu zako wengine.
Hii ni sawa na mawingu kabla ya mvua. Kwa sababu kama atashindwa kuwajali ndugu zako japo kwa kuwajulia hali wakati huu, utakapoingia katika ndoa atakuruhusu ukawasabahi kweli?
Rafiki zangu, zipo sifa nyingi sana za kuangalia lakini hizi ni zile muhimu zaidi, ambazo kama mwanaume wako anazo, basi ni ruksa kumpa moyo wako wote. Mada imeisha.
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi ambaye anaandikia magazeti ya , ameandika vitabu vya True Love na Let’s Talk About Love. Unaweza kumtembelea kwenye mtandao wake; HYPERLINK “
No comments:
Post a Comment